Mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint Germain ‘PSG’ wameendelea na mpango wa kuhitaji saini ya kiungo kutoka nchini England na klabu ya Totten Hotspurs Dele Alli kwa mkopo.
Taarifa kutoka nchini England zinaeleza kuwa, maafisa wa PSG wapo jijini London wakiendelea na mazungumzo, lakini uongozi wa Spurs wameonesha kutokua tayari kumuachia Alli, pasina kufanikisha harakati za kumpata mbadala wake.
Klabu hizo mbili zimekuwa kwenye mazungumzo kwa siku kadhaa, na dhamira kubwa ya PSG ni kutaka kumpeleka kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa meneja wake wa zamani Mauricio Pochettino aliekabidhiwa benchi la ufundi huko Parc des Princes.
Christian Eriksen, ambaye amekuwa na wakati mgumu tangu alipojiunga Inter Milan akitokea Spurs, amekua chaguo la kwanza la Jose Mourinho, katika hatua za kuziba nafasi ya Alli, lakini wababe wa Milan wamewasilisha ombi la kujizua jukumu la kumlipa mshahara, katika kipindi chote ambacho atarejea England kwa mkopo.