Jumla ya watu 16 wamepoteza maisha katika mji wenye migodi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa.
Kwa mujibu wa Maafisa wa usalama eneo hilo wamesema, ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia Jumanne katika mji wa Kamituga kwenye mkoa wa Kivu Kusini huku Kaimu meya wa mji huo, Alexandre Ngandu akisema wanawake na watoto ni miongoni mwa waliokufa.
Mkuu wa shirika la kiraia la Kamituga, Tristan Mukamba Mwanga amesema vitongoji vinne vya mji huo vimeathirika, lakini vifo vingi vimetokea katika makazi ya mabanda yaliyojengwa bila vibali kwenye eneo la mteremko.
Hata hivyo, wakaazi wa Kamituga wamearifu kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa mbele ya jengo la ofisi za mji tayari kwa mazishi ambapo wiki iliyopita, watu wengine 20 walikufa katika Wilaya ya Masisi iliyopo Mkoa wa Kivu Kaskazini, kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo.