Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa yasiyoambukiza, Afya ya Akili na Ajali kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Omary Ubuguyu amesema haipaswi kumzuia mtu anayelia kwani husaidia kumrejeza katika hali ya kawaida, kauli ambayo ameitoa wakati akibainisha mbinu tofauti ikiwemo michezo mbalimbali itakayotumika kuwajenga Kisaikolojia Wanafunzi shuleni kutokana na athari za mafuriko Wilayani Hanang’.
Akizungumza mara baada ya kutolewa mafunzo hayo Mjini Katesh Wilayani Hanang Mkoani Manyara, Dkt. Ubuguyu amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana Shirika la Save the Children tayari imetoa Mafunzo kwa takriban Walimu 30 kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kutoa Msaada wa Kisaikolojia shuleni.
Amesema, “watu wengi waliumizwa hivyo wanapolia kuonesha hisia zao tuache walie inawasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida na pia mtu anayetaka kujiua tunaomba haraka tuwasiliane kwa ajili ya msaada wa Kisaikolojia na watu wanaotumia pombe kama sehemu ya kukabiliana na changamoto ya mafuriko ni muhimu pia kuwasaidia huduma za Kisaikolojia.”
Kuhusu mafunzo hayo, Dkt. Ubuguyu amesema “yatasaidia walimu kuweza kutoa huduma za Kisaikolojia kwao binafsi na watoto watakapofungua shule mwezi Januari, kwa bahati mbaya wapo watoto ambao tumewapoteza au kupoteza ndugu kwa hiyo kabla ya kufika Januari tumeanza kutoa mafunzo kwa walimu, ili kuwa na uwezo wa kutoa msaada ya Kisaikolojia.”
Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya Walimu kutoka katika kata zilizoathirika na mafuriko Wilayani Hanang Mkoani Manyara wamesema mafunzo ya Saikolojia waliyopata kutoka kwa Watalaam kutoka Wizara ya Afya yatawasaidia kuwaweka katika hali ya kawaida Wanafunzi.
“Mafunzo haya yatatusaidia kukaa vizuri na wanafunzi na namna ya kuwajenga Kisaikolojia maana unakuta mwanafunzi alikuwa na wazazi ama walezi wake lakini atakapofungua shule utakuta hana rafiki aliyekuwa anakaa naye karibu hivyo mafunzo haya yana umuhimu sana kwetu,” wamesema.