Mshambuliaji wa Klabu Bingwa nchini England Manchester City, Erling Haaland, amechaguliwa kuwa mwanamichezo bora wa Dunia wa Shirika la Utangazaji la Uingereza ‘BBC’.

Haaland ameshinda tuzo hiyo, baada ya kuisaidia klabu yake Man City kutwaa mataji matatu ‘Treble’ msimu uliopita 2022/23.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, raia wa Norway, alifunga mabao 52 katika mashindano yote msimu uliopita, wakati City ikitwaa mataji ya Ligi Kuu ya England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA.

“Ahsante sana kwa kunipigia kura kuwa mwanamichezo nyota bora wa mwaka wa BBC. Msimu uliopita ulikuwa mzuri sana, nilishinda mataji matatu na tulifanya vizuri sana.” amesema.

Tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka wa dunia ya BBC hupigiwa kura na wasomaji wa tovuti ya michezo ya BBC Sport.

Katika tuzo hiyo, Nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, iliyoshinda Kombe la Dunia la mchezo wa Rugby, Siya Kolisi, alishika nafasi ya pili huku mshindi wa dunia wa mbio za magari za Formula 1, Max Verstappen, akishika nafasi ya tatu.

Neymar awekwa pembeni Copa America
Usimzuie mtu anayelia, kilio kinamsaidia - Dkt. Ubuguyu