Mshambuliaji nyota wa Brazil, Neymar atazikosa Fainali za Mataifa ya Kusini kwa Amerika ‘Copa Amerika’ zitakazofanyika nchini Marekani kutokana na majeraha aliyoyapata mwezi Oktoba, alithibitisha daktari wa timu ya taifa ya Brazil, Rodrigo Lasmar.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 wa Al Hilal aliumia kwenye mchezo wa kufuzu wa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Uruguay Oktoba 17 na kufanyiwa upasuaji wiki mbili baadaye. Mashindano ya Copa Amerika yataanza Juni 20 na yatamalizika Julai 14.

“Ni mapema sana. Hakuna sababu ya kuruka hatua za kupona kwake na kumuingiza kwenye hatari zisizo za lazima. Matarajio yetu atarejea mwanzoni mwa msimu mpya mwaka 2024 ambao utakuwa mwezi Agosti.

“Tunatakiwa kuwa wavumilivu. Kuzungumzia kurejea kwake kabla ya miezi tisa ni mapema. Ni muhimu sana kuheshimu muda wa madaktari, muda ambao mwili utajiunga tena.

“Kama tunafuata hatua zote na baada ya muda mrefu wa kupona, matarajio ni kwamba anaweza kupona vizuri kabisa.” Alisema Rodrigo Lasmar

Neymar ni mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Brazil akiwa amefunga mabao 79 kwenye mechi 129.

Guardiola anautaka ubingwa wa dunia
Erling Haaland atwaa tuzo ya dunia