Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema endapo zao la Zabibu litasimamiwa vizuri, ikatolewa elimu ya kutosha na likawepo soko la uhakika, litawawezesha Wakulima kumudu maisha, kwani lina sehemu mbili zenye faida ambazo ni Matunda na Mvinyo.

Pinda aliyasema hayo katika mahojiano maalum aliyowahi kuyafanya na Dar24 Media Kijijini kwake Zuzu anapofanya shughuli za Kilimo, na kusema jitihada za Serikali za kulitazama zao hilo kibiashara na lenye kuinua uchumi ni wazi zitasaidia kuboresha kipato cha mtu mmoja mmoja kibiashara na pato la Taifa.

Amesema, “na niishukuru tu Serikali ya Mkoa (Dodoma), imelivaa hili kama jambo la msingi na tunaamini kabisa zao la Zabibu likisimamiwa vizuri, elimu ya kutosha ikawepo tukawa na soko la uhakika lenye bei nzuri, Zabibu ni zao ambalo linamuwezesha mtu kumudu maisha.”

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Pinda amesema zao la Zabibu ni la kimkakati kwa Mkoa wa Dodoma na ndio maana ilianzishwa Kampuni ya Dodoma Wine – DOWICO, ambayo ilikuwa maalum kwa Zabibu za Mvinyo pekee, hivyo uendelezaji wa Kilimo hicho utasaidia kuongeza tija katika shughuli za kibiashara.

“Na ndio maana unaona hata baada ya kutoweka kwa Dowico bado mvinyo uliendelea kutengenezwa na Kilimo kiliendelea na uzuri (Zabibu), inalika kwasababu inapokuwa kwenye joto la kutosha inatengeneza Sukari ya kutosha ingawa uchachu bado utakuwepo,” amefafanua Pinda.

Hata hivyo, Pinda amesisitiza umuhimu wa kupenda kulima badala ya kununua mazao kwa ajili ya chakula, akitolea mfano kuwa, “mimi natoka Katavi na chakula chetu kule ni ugali, tuliona haina haja ya kununua mahindi na badala yake tunalima mahindi tunakoboa tunapata unga na mboga mboga tunalima wenyewe.”

Chasamba: Nguvu zilinipa ajira, ukaribu na Rais
Ujenzi wa Barabara Tanga - Pangani wafikia asilimia 74