Rais wa Klabu bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said amesema anataka kuiona klabu hiyo inakuwa katika orodha ya Klabu nne Bora Barani Afrika kuanzia msimu ujao 2024/25.

Young Africans ambayo kwa sasa inakaribia kutetea ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara yatatu mfululizo, ilifika hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kutolewa na Mabingwa wa Soka Afrika Kusini Mamelodi Sundowns kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati mwanzoni mwa mwezi huu.

Akizungumza jijini Dar es salaam leo Jumatatu (Aprili 29), Hersi amesema anaamini kwa ubora wa kikosi cha Young Africans kwa sasa, ndio maana ameweka mipango ya kuhakikisha wanakuwa katika orodha ya Klabu nne Bora Barani Afrika.

Amesema mpango huo unawezekana kwa sababu katika ushindani wa ndani ya Tanzania hakuna klabu yenye kikosi chenye ubora kama Young Africans, na ndio maana kila mpinzani wanayekutana naye hucheza kwa kujihami.

“Kwa sasa hakuna Klabu Tanzania inayoweza kuisogelea Young Africans SC kwenye ubora. Ndio maana timu nyingi zikicheza na sisi zinakuja na mfumo wa kuzuia zaidi ikimaanisha wanaiheshimu Klabu yetu. Malengo yangu makubwa ni kuhakikisha Klabu yetu inakuwa moja ya Klabu bora Afrika.

“Na matamanio yangu ni kuona mwakani kwenye mashindano ya Kimataifa tufike katika orodha ya timu nne bora AFRIKA, ili tuweze kushiriki Kombe la Dunia la Vilabu. Mwaka jana tumefika fainali na tumepata alama nyingi ambazo zitatuongezea nguvu ya kushiriki Kombe hilo” amesema Hersi Said

Kiongozi huyo amekuwa sehemu ya viongozi walioweka alama klabuni hapo baada ya kuwa sehemu ya mafanikio ya Young Africans ambayo ilikwama kucheza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini uongozi wake ulifanikiwa kufika hatua hiyo msimu huu 2023/24 na kucheza Robo Fainali.

 

Mohameed Salah: Ukimya wangu una maana kubwa
Gamondi apotezea Ubingwa Ligi Kuu