Baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad Casablanca kutoka Morocco, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, amewapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango kizuri na kuongeza bado hawajamaliza kazi.
Simba SC ambayo imefikisha pointi tano na kupaa hadi katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, imebakiza mechi mbili ambapo itaifuata ASEC Mimosas huko Ivory Coast na itamaliza hatua hiyo kwa kuikaribisha kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jwaneng Galaxy kutoka Botswana.
Benchikha amesema, Simba SC inahitaji kuendelea kufanya vyema katika mechi zake nyingine mbili zilizobakia ili kufikia malengo ya kusonga mbele katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoendelea.
Kocha huyo amesema ana imani kubwa na kikosi chake na anaamini kina uwezo wa kufanya vizuri ili kucheza hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo.
Amesema mechi hiyo ilikuwa ya ushindani na kila timu ilicheza vizuri lakini amewapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo aliyowapa kwenye uwanja wa mazoezi.
“Wachezaji walifanya kazi nzuri, tulifanya mashambulizi na kufunga lakini hatukuruhusu bao, kipindi cha pili Wydad walitawala eneo letu, walifanya mashambulizi na kubadilisha mfumo kwa kuongeza mabeki.
Nafasi ya kwenda Robo Fainali ipo wazi, kazi iliyopo kwetu ni kujiandaa na michezo miwili iliyosalia ambayo tunahitaji ushindi ili kujihakikishia safari yetu ya kucheza Robo Fainali,” amesema Benchikha.
Ameongeza baada ya mechi hiyo wanarejea kwenye uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza ili kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi KUU Tanzania Bara dhidi ya KMC FC utakaochezwa keshokutwa Jumamosi (Desemba 23).
Naye mfungaji wa mabao yote katika mechi hiyo, Willy Essomba Onana, amesema Benchikha amempa morali na ari ya kujituma kufanya vizuri kutokana na kumwamini.
“Huu ushindi ni wetu wote, niwapongeze wachezaji wenzangu, tumepambana kusaka ushindi, lakini pia mashabiki wa Simba SC wanatakiwa kuwa wakweli, tunapokuwa katika wakati mgumu na furaha tuungane pamoja,” amesema Onana.