Benchi la Ufundi la Young Africans limesema litatumia nguvu ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kuikabili Tabora United katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho Jumamosi (Desemba 23) kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans watawavaa wenyeji Tabora United ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mabao 3-0 walioupata dhidi ya Medeama SC kutoka Ghana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afirika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam juzi Jumatano (Desemba 20).
Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, amesema tayari wameshasahau mnatokeo ya mechi iliyopita ya mashindano ya kimataifa na sasa wanageuza silaha zao kuhakikisha wanaenda kupambana kupata ushindi dhidi ya Tabora United.
Gamondi amesema baada ya kumaliza mechi hiyo, kikosi chake kilirejea kwenye uwanja wa mazoezi na kufanyia kazi mapungufu waliyoyabaini kwa ajili ya kuhakikisha wanaenda Dodoma kuchukua alama tatu muhimu.
Kocha huyo amesema kila mchezo una mipango yake na Young Africans imejipanga kuingia tofauti katika mechi ya kesho Jumamosi (Desemba 23) dhidi ya timu hiyo mpya iliyopanda daraja msimu huu.
“Tunaenda kukabiliana na Tabora United kwa mbinu nyingine, tunataka kuendeleza ushindi katika michezo yetu ya Ligi Kuu ingawa nafahamu mchezo hautakuwa mwepesi kutokana na ratiba ya timu yangu.” amesema Gamondi.
Kocha huyo amesema wachezaji wake lazima wakapambane na kujituma licha ya uchovu walikuwa nao baada ya kutoka kucheza mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Nina imani na wachezaji, kwetu kikubwa ni ushindi, tutacheza na Tabora United huku tukiwa na lengo moja tu la kusaka ushindi, tutapambana kufanikisha hili.” amesema Gamondi.
Meneja wa timu hiyo, Harrison Walter, amesema maandalizi kuelekea mechi hiyo yako katika hatua za mwisho na wamejipanga kuendelea kuwapa furaha mashabiki na wanachama wao.
Walter amesema kila mechi kwao ni sawa na fainali kwa sababu wanahitaji kukusanya alama tatu muhimu na hatimaye kurejea katika kilele cha msimamno wa ligi hiyo.
Tumejipanga kwenda kupambana, hakuna mechi rahisi, kila mchezaji wa Young Africans anafahamu hilo, hatutabweteka na matokeo ya mechi yetu iliyopita ya CAF, tunawaheshimu wapinzani wetu,” meneja huyo amesema.
Young Africans itashuka dimbani kesho Jumamosi (Desemba 23) ikiwa pia na kumbukumbu ya kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Mabingwa hao watetezi wana alama 27 kibindoni na wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara nyuma ya vinara, Azam FC yenye pointi 31, lakini Young Africans wakiwa na michezo miwili mkononi.
Simba yenye alama 22 lakini imeshuka dimbani mara tisa itacheza mechi yake nyingine ya ligi hiyo yenye kushirikisha timu 16 kesho Jumamosi (Desemba 23) dhidi ya KMC FC.