Michezo saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeahirishwa ili kupisha mchezo kati ya timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ dhidi ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ utakaofanyika Desemba 27 na maandalizi ya timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars’.
Taifa Stars inajiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zitakazofanyika Ivory Coast kuanzia Januari 13, mwakani.
Mchezo huo maalumu utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar utatumika kufungua uwanja huo baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Zanzibar ‘SMZ’.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), michezo iliyoahirishwa ni ile ambayo ilikuwa ichezwe kuanzia Desemba 29 hadi Januari 2, 2024 ambayo ni Tabora United vs Simba SC, Young Africans vs Mashujaa FC, Mashujaa FC vs Simba SC.
Michezo mingine ni Kagera Sugar vs Young Africans, Simba SC vs Azam FC, Geita Gold vs Simba SC na Young Africans vs Dodoma Jiji.
Michezo tajwa hapo juu iliyoahirishwa itapangiwa tarehe nyingine baada ya Taifa Stars kumaliza michuano ya AFCON 2023.