Beki wa Forfar, Roberto Nditi amekiri kuwa na furaha isiyo na kifani kutoka kucheza katika Uwanja wa Peterhead, League Two ya Scotland na kukabili kikosi cha taifa cha Morocco katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).
Nditi mwenye umri wa miaka 23, ameteuliwa katika kikosi cha Tanzania kitakachoshiriki Afcon 2023 nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13, mwakani.
Mechi ya kwanza ya hatua ya makundi, Taifa Stars itacheza dhidi ya Morocco Januari 17.
“Hakika huu ni wakati muhimu sana kwangu na kwa familia yangu. Siwezi kusubiri kufanikisha hili,” amesema wakati akizungumza na mtandao wa soka wa Scotland.
“Ni fursa ambayo sikuwahi kufikiria ingekuja lakini imekuja na siwezi kukataa. Ukitafakari kwa kina, inashangaza kweli! Yaani kutoka Peterhead Jumamosi moja na kwenda kucheza na moja ya timu bora kabisa duniani, Morocco
Nditi anasema kwa kucheza dhidi ya wachezaji wa juu katika Afcon kutaimarisha kiwango chake mwenyewe.
Nditi atajiunga na kikosi cha Taifa Stars chenye Mshambuliaji wa zamani wa Aston Villa, Mbwana Samatta, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya PAOK Salonika ya Ugiriki.
“Utakuwa uzoefu mzuri na nitajifunza kutoka kwa wachezaji wengine, kila mtu ana ubora wa hali ya juu,” ameongeza Nditi.
Nditi ambaye ni Mtanzania kutokana na wazazi wake, anajiunga na wenzake wa kimataifa Desemba 26, mwaka huu na atakuwa Afrika hadi mwishoni mwa Januari 2024.
Tanzania inayoshika nafasi ya 121 katika viwango vya FIFA, ina mchezaji mwingine Haji Mnoga anayechezea timu ya Aldershot Town, England.
Hii ni mara ya tatu kwa Taifa Stars kushiriki AFCON 2023 na wako Kundi F pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Morocco yenye nyota kibao.