Jumla ya Madereva 14 wa magari ya IT wamekamatwa Mkoani Morogoro kutokana na kosa la kubeba abiri kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.
Kukamatwa kwa madereva hao kumetokana na doria inayoendelea kufanywa na Mwanasheria wa Kikosi cha usalama barabarani, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Deus Sokoni akiwa na Mkaguzi wa Polisi, Faustina Ndunguru, Sajenti Erasto na koplo Rashidi katika barabara kuu ya Morogoro – Iringa.
SSP Sokoni alimuagiza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilaya ya Ruhembe, ASP Julius Mangure kuhakikisha madereva hao wanachukuliwa hatua za kisheria na abiria waliokuwa wamewabeba kwenye magari hayo watafutiwe usafiri mwingine ambao utakuwa ni salama kwao.
Aidha, kwa upande wa madereva wa mabasi wametakiwa kuendesha kwa kujihami na kuchukua tahadhari wakati wote wawapo safarini, sambamba na kuachana na matumizi ya vilevi na pia madereva wa magari ya mizigo kuhakikisha wanaegesha vizuri magari katika eneo la maegesho.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa abiria wote kutumia usafiri wa mabasi ambayo Serikali imeruhusu kusafiri masaa 24, hivyo abiria hawana sababu za kusafiri kwa magari ya IT ambayo ni hatari kwao.