Bila shaka umewahi kumuona mlemavu wa macho, mara nyingi watu wa aina hii huwa na hisia za ajabu na matendo yao hushangaza kiasi yanaweza kukupa hofu juu yao lakini ukichunguza utakuja pata tabasamu kwa jinsi ambavyo mtu huyo eidha alipiga hesabu au alifanikisha lengo ambalo wewe hukudhani kutokana na tatizo alilonalo.
Kuna kisa kimoja aliwahi kukiandika Mwandishi wangu wa wakati wote (Role Model), Maundu Mwingizi (Mwanabalagha), kuhusu hekima za Mlemavu mmoja wa macho jinsi alivyowashangaza wafuatiliaji wa mambo.
Mwingizi aliasimulia katika andiko lake kuwa hapo kale, katika mji mmoja mdogo, alipata kuishi bwana mmoja Mlemavu wa macho na cha ajabu, kila alipokuwa akitoka nje wakati wa usiku, alitoka na taa (chemli), ikiwa imewashwa.
Siku moja usiku, akiwa anatoka msalani na taa yake mkononi, mmoja kati ya Vijana wengi waliokuwa wakishangazwa na jambo hilo alimsaili, “Mzee naomba kukuuliza. Sote twajua wewe ni kipofu, hauna uwezo wa kuona chochote. Sasa kwanini kila utokapo nje wakati wa usiku, unajitaabisha kubeba taa?”
Bwana yule Mlemavu wa macho akamjibu, “ni kweli siwezi kuona kwa sababu ni kipofu. Lakini nalazimika kutembea na taa kwa sababu yenu wenye kuona. Macho yamewalaghai akili kiasi cha kuamini mnaweza kuona hadi vya gizani. Na kwa sababu hiyo, mnaweza kutupamia na kutudhuru siye tusioona kama hatutokumulikieni taa!”
Maundu anamalizia andiko lake kwa kusema Vijana wale wakamtaka radhi mzee yule, na kumshukuru kwa somo mujarabu alilowaachia. Sina shaka nawe umeambua kitu kwamba wakati mwingine tunalazimika hata kukohoa bila kuwa na kikohizi ili watu wafahamu kuwa tupo maana ukimya wako waweza kuwa tatizo kwako ukakuletea shida.