Mshambuliaji Simon Msuva yupo nchini tayari baada ya kutua nchini kimyakimya, kuwahi kambi ya timu ya taifa inayojiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), lakini akianzia kambi ya timu ya Kilimanjaro Stars ya Bara itajayocheza na Zanzibar Heroes katika mechi maalumu ya kirafiki mjini Unguja.

Msuva ametua, huku mabosi wa Young Africans wakiendelea na mazungumzo naye ili kumsainisha, lakini hapo hapo mabosi wa klabu hiyo wakalazimika kufumua mahesabu yao ndani ya dili hilo.

Young Africans inaamini kama itampata Msuva, aliyeachana na JS Kabylie ya Algeria utakuwa usajili muhimu ndani ya kikosi hicho wakitafakari juu ya ubora alionao mshambuliaji huyo wa zamani wa timu hiyo.

Msuva tayari ameonyesha kuingia kwenye laini ya Young Africans akiwataka kusubiri atue nchini ili aongee na familia yake kwanza kwa kina kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho ya kurejea Jangwani ikiwa ni baada ya kuondoka mwaka 2017 kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi akianzia Morocco kisha Saudia Arabia halafu Algeria.

Young Africans imemuwekea fedha ya kufuru mezani ambayo imemfanya ajiulize mara mbili kabla ya kuamua wapi atue, ingawa mshambuliaji huyo akili yake ikitamani kuendeleca kucheza nje.

Kama Young Africans ikimnasa Msuva, klabu hiyo inaona ni bora isajili mshambuliaji mmoja pekee wa kigeni na badala yake wahamishie nguvu eneo lingine wakitaka kumshusha winga wa maana.

Rekodi za Msuva zimekubalika pia kwa Kocha Miguel Gamondi akiwaambia kwa kifupi mabosi wa klabu hiyo kwa kuwaambia; “Nileteeni tu, atatufaa hapa.” maneno ambayo ni kama yamewafanya viongozi kuingiza gia kubwa kukimbizana na usajili huo.

Young Africans haitaki kufanya makosa kwa Msuva kabla hakapanda ndege ya kwenda Ivory Coast na kikosi cha Taifa Stars.

“Unajua hii ni mara ya pili kama sio ya tatu tunarudi kwake, kwa namna hawa Waarabu walivyomfanyia ni bora sasa akarudi kwanza kutuliza akili hapa kwetu, kwa kuwa ameshafika acha tusubiri kuona nini ataamua na familia yake” amesema bosi mmoja wa juu.

Mbali na Msuva, Young Africans inahusishwa na Washambuliaji Jonathan Sowah wa Medeama SC ya Ghana, Ranga Chivaviro wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Sankara Karamoko wa Ivory Coast.

Pia, inamzengea Moses Phiri anayedaiwa kuandika barua yakutaka kuondoka Simba SC.

Kichuya kuibukia JKT Tanzania
Uchaguzi DRC: Tshisekedi aongoza matokeo ya awali