Wakati timu ya taifa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Zanzibar Heroes zikishuka dimbani, makocha wa timu hizo wametamba kuviongoza yema vikosi vyao kupata ushindi.
Timu hizo zitavaana leo Jumatano (Desemba 27) saa 2:15 usiku katika mchezo maalumu wa kirafiki wa kuzindua Uwanja wa Amaan uliopo kisiwani Unguja, Zanzibar.
Wakizungumzia mchezo, makocha wa timu hizo wametamba kuwaongoza vyema wachezaji wao kuonyesha soka la ushindani na kupata ushindi.
Kocha wa Kilimanjaro Stars, Adel Amrouche, amesema mchezo huo utakuwa ni moja ya kipimo bora kwa wachezaji wake kabla ya kutaja kikosi cha mwisho cha timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, zitakazofanyika lvory Coast mwakani.
Amrouche amesema pamoja na kupata muda mchache wa kukinoa kikosi hicho, lakini anaamini wachezaji wake watafuata vyema maelekezo yake na kupata ushindi katika mechi hiyo.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema atautumia vyema mchezo huo kujua ubora na mapungufu ya wachezaji aliowaita kikosini.
“Huu ni mchezo muhimu kwetu kwani utanisaidia kuona wapi katika kikosi kina mapungufu, tunakwenda kwenye fainali za ‘AFCON 2023’ huko kuna timu imara hivyo bila ya kujipanga vizuri hatuwezi kufika mbali,” amesema.
Naye Kocha wa Zanzibar Heroes, Hemed Morocco, amesema amejipanga vizuri kukiongoza kikosi chake kuonyesha kupata ushindi.
Amesema anawafahamu vizuri wachezaji wa Kilimanjaro Stars hivyo anaamini utakuwa mchezo wenye ushindani mkubwa, lakini atahakikisha kikosi chake kinashinda.
“Huu ni mchezo muhimu sana kwetu na kipimo bora kwa timu yangu, naamini wachezaji watatumia vyema mbinu nilizowapatia,” amesema.
Baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Kilimanjaro na Taifa Stars, Amrouche atakuwa na kibarua cha kuchagua kikosi cha wachezaji 27 kabla ya Januari 03, 2024 kwa ajili ya ‘AFCON 2023’.
Katika Fainali za AFCON 2023, Taifa Stars imepangwa Kundi F na timu za Morocco, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.
Juma lililopita Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, liliweka wazi kikosi cha awali cha Taifa Stars chenye wachezaji 53 kilichoitwa na Kocha Amrouche kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Bara hilo ‘AFCON 2023’.
Katika kikosi hicho, Amrouche amewajumuisha wachezaji Pellegrino Ahmal (Bodo-Sweden), Adam Diokas Kasa (IFK Haninge-Sweden), Adolf Bitegeko (Volsungur IF-lceland), Tarryn Allarakhia (Wealdstone-Uingereza), Miano Danilo (Telford United-Uingereza), Mohamed Sagaf (Boreham Wood-Uingereza) na Twarig Ahmed (Telford United-Uingereza).
Wachezaji wengine wanaounda kikosi hicho cha awali ni Beno Kakolanya (Singida Fountain Gate), Aishi Manula (Simba), Aboutwalib Mshery, Metacha Mnata, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, lbrahimn Abdallah Hamad, Nickson Kibabage (Young Africans), Lusajo Mwaikenda (Azam FC), (Yanga), Haji Mnoga (Aldershot Town), Abdi Banda (Richards Bay), Zion Nditi (Aldershot Town), Novatus Dismas (Shakhar Donetsk) na Edwin Balua (Tanzania Prisons).
Wengine ni Abdulmalik Zakaria (Namungo), Omar Mvungi (FC Nantes), Mzamiru Yasin (Simba), Sospeter Bajana (Azam FC), Baraka Majogoro (Chippa United).
Feisal Salum (Azam FC), Mudathir Yahya (Young Africans), Morice Abraham (RFK Novi Sad), Himid Mao (Talaea El Gish), Ladaki Chasambi (Mtibwa Sugar), Mbwana Samatta (PAOK) na Saimon Msuva (JS Kabylie).
Roberto Nditi (Forfar Athletic), Kibu Denis (Simba), Abdul Suleiman (Azam FC), Ben Starkie (Basford United), Matheo Anton (Mtibwa Sugar), Charles Mmombwa (Macarthur), Joshua lbrahim (Tusker FC), Clement Mzize (Young Africans), Mohamed Hussein (Simba), Kennedy Juma (Simba) na Ayoub Bilali (FK Gorazde).
Wengine ni Khleffin Hamdoun (Muscat club), Israel Mwenda (Simba), Adam Salamba (Ly stade club), Elias Lawi (Coastal Union), Said Khamis (FK Jedinstvo) Yusuph Kagoma (Singida Fountain Gate) na Cyprian Thobias Kachwele.