Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa kirafiki wa timu ya soka ya Tanzania Bara dhidi ya Zanzibar Heroes utakaochezwa Uwanja wa Amaan, Unguja leo Jumatano (Desemba 27).
Mchezo huo ambao ni maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa uwanja huo baada ya ukarabati mkubwa unatarajiwa kuanza saa 2:15 usiku na mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa kwenye michuano ya CECAFA, iliyounguruma nchini Uganda na Kili Stars ilishinda 1-0.
Akizungumzia mchezo huo Kodha Mkuu wa Taifa Stars, Adel Amrouche amesema atautumia mchezo huo kupata kikosi kitachoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 mwakani.
“Naupa umuhimu mkubwa mchezo huu wa kirafiki dhidi ya Zanzibar. Utanisaidia kufanya mchujo kupata wachezaji ninaowahitaji. Kila mchezaji atakayepata nafasi kucheza anapaswa kuupa umuhimu mkubwa mchezo huu,” amesema Amrouche.
Naye Nahodha na Beki wa Kilimanjaro Stars, Bakari Mwamnyeto amewaita mashabiki na kusema: “Njooni muone wachezaji wageni lakini wageni kwa kucheza, utakuwa mhezo mzuri maana wachezaji tunajuana.”
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Zanzibar Heroes, Salehe Machupa amesema hakuna mchezaji atakayekosa mchezo huo japo ni mechi ya sherehe na tunadheza na ndugu zetu lakini hatutakubali kufungwa.
Nyota wa Zanzibar Heroes, Feisal Salum Fei Toto’ amesema waanawaheshimu wapinzani wao kwani ndugu zao japo wana wachezaji wazuri na wazoefu lakini hawatakubali kufungwa kwa mara ya pili.
Hatutaki kuwaangusha Wazanzibar katika uwanja wa nyumbani japo wenzetu wana kikosi bora hatutakubali kufungwa mara ya pili,” amesema Fei Toto.