Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema ushindani kwenye Ligi Kuu msimu huu ndio chanzo cha makocha wengi kufukuzwa kazi.
Maxime alifutwa kazi juma lililopita kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye ligi pamoja na vipigo vikubwa kutoka kwa Simba SC na Azam FC.
Kocha huyo amesema timu nyingi msimu huu zimejipanga vizuri ikiwemo kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa ushindani.
“Fukuza fukuza ya makocha msimu huu ni ishara kwamba ligi yetu ushindani umeongezeka na viongozi wanayo haki ya maamuzi kama wanaona mambo hayaendi sawa kulingana na makubaliano yao,” amesema Maxime.
Hata hivyo Maxime amesema pamoja na makocha wengi kufukuzwa haimaanishi hawana uwezo bali ni upepo mbaya wa kukosa matokea mazuri umewapitia.
Maxime amesema yeye binafsi anaamini ana uwezo mkubwa isipokuwa changamoto za hapa na pale ndio zimesababisha akashindwa.
Hiyo ni mara ya pili kwa Maxime kufutwa kazi Kagera Sugar, mara ya kwanza ilikuwa misimu miwili iliyopita na nafasi yake kuchukuliwa na Francis Baraza raia wa Kenya.