Lydia Mollel – Morogoro.
Operesheni mbalimbali zinazoenedelea kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, zinaendelea kuzaa matunda kwani limefanikiwa kumakamata Athumani Juma (33) mkazi wa eneo la Mdizini Tarafa ya Turiani Wilaya ya Mvomero kwa kosa la kumbaka binti wa miaka 12 ambae pia ni mwanafunzi wa darasa la tano na kumuambukiza virusi vya ukimwi.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Morogoro, Alex Mkama ambaye amesema Jeshi la polisi kwa kushirikiana na Wananchi wa Mdizini kwa pamoja walimtafuta Juma na kumkamata kisha kumfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Mvomero.
Kamanda Mkama amesema, baada ya Mtuhumiwa huyo kufikishwa Mahakamani alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka na miaka 5 kwa kosa la kumuambukiza virusi vya Ukimwi, binti huyo.
Hata hivyo, historia inaonesha mtuhumiwa huyo si mara ya kwanza kutenda makosa hayo, kwani aliwahi kufanya kosa kama hilo mwaka 2020 kwa kubaka Watoto wawili wenye umri wa miaka 9 na 11 na kufikishwa mbele ya Mahakama ya wilaya ya Mvomero kisha kutoka kwa rufaa
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeendelea na operesheni ya misako mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa kipindi chote cha mwezi Desemba 2023, ili kuhakikisha Morogoro na maeneo yake yanakuwa salama.