Uongozi wa Azam FC, umesema kuwa umeridhishwa na uwezo na kiwango cha mshambuliaji wao mpya, Franklin Navarro ambaye amejiunga na kikosi cha timu hiyo, visiwani Zanzibar.
Azam FC tayari wamemtambulisha usajili wao wa kwanza ambaye ni mchezaji Navarro mwenye umri wa miaka 23 akitokea Ligi Daraja la Pili nchini Colombia, amefunga bao moja na kutoa pasi mbili za mwisho katika mechi 14.
Akizungumza kisiwani Unguja-Zanzibar, Ofisa Habari wa Azam FC, Hashim lbwe amesema hawana mashaka kabisa na uwezo wa mchezaji huyo wakiamini atawasaidia kufikia malengo yao katika mashindano yaliyopo mbele yao.
Amesema mchezaji huyo amejiunga na timu visiwani Zanzibar jana na atakuwa sehemu ya mipango ya benchi lao la ufundi linaloongozwa na makocha Youssouph Dabo na Bruno Ferry katika michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi.
“Mkataba wake ni siri kati yetu mchezaji pamoja na mtu anayemsimamia, hii ni kupunguza presha kwa nyota wetu, tuna imani na mchezaji huyo na hatutaki kumpa presha kulingana na rekodi aliyonayo.
“Anaweza kucheza nafasi nyingi ikiwemo Kiungo Mshambuliaji, winga pia Mshambuliaji halisi ambaye ndiyo namba yake, mchezaji anayetoka katika ligi ya Colombia ni ligi yenye daraja kubwa, ukiangalia kuna baadhi ya timu kutoka Afrika Kusini na mabara mengine Ulaya wanasajili kutoka nchini hiyo na sisi Azam FC safari hii tumeenda huko pia,” amesema Ibwe.
Amesisitiza kuwa bado wanaendelea kufanya usajili kwa kuongeza vifaa kwa lengo la kuongeza nguvu katika timu yao na hivi karibuni wanatarajia kushusha vifaa vingine ambavyo vitaenda kuongeza nguvu kikosini visiwani humo.
“Tunahitaji kufanya usajili mapema na kuwahi katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa sababu ya kutaka kuwapa muda wa kuzoeana lakini kutowapa presha wachezaji wetu hao watakaporejea katika ligi,” amesema lbwe.
Kuhusu mipango yao Kombe la Mapinduzi, amesema ni kucheza Fainali za michezo hiyo na kuhakikisha wanafanikiwa kutwaa taji la ubingwa, kwa sababu wanahitaji mechi ya pili kwenda na kasi yao yaliyotoka nayo katika michezo ya ligi kuu.