Mlinda Lango kutoka nchini Cameroon Andre Onana yuko katika mazungumzo na Chama cha Soka cha nchi hiyo ‘FECAFOOT’ ili kujaribu kucheleweshwa kujiunga kwake kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, kwa mujibU wa ESPN.

Kipa huyo wa Manchester United ameitwa katika kikosi cha Cameroon kuelekea Fainali hizo zitakazoanza Januari 13, mwakani nchini Ivory Coast.

Onana, aliyesajiliwa kwa Pauni Milioni 43 majira ya joto kutoka Inter Milan ameonyesha atashiriki lakini, kwa mujibu wa ESPN anataka kupunguza muda wake nje ya Old Trafford kadri awezavyo.

Cameroon wanatarajiwa kuweka kambi nchini Saudi Arabia, ambapo watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Zambia Januari 9, mwakani.

Hata hivyo, Onana ana nia ya kuichezea United katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Wigan Athletic kwenye Uwanja wa DW Januari 8, mwakani wakati Cameroon itaanza kampeni yake ya AFCON dhidi ya Guinea Januari 15.

Raundi ya mtoano itaanza Januari 27 huku fainali ikipangwa Februari 11, mwakani.

United wana mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Hotspur Januari 14, mwakani na uwezekano wa mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA mnamo Januari 27 na 28 kabla ya mechi za Ligi Kuu dhidi ya Wolves Februari Mosi, West Ham United Februari 4 na Aston Villa Februari 11, mwakani.

Onana alistaafu kucheza mechi za kimataifa wakati wa Kombe la Dunia nchini Qatar kabla ya kurejea Septemba, mwaka huu.

Pindi tu atakapojiunga na kikosi hicho cha Kocha Rigobert Song kwa ajili ya AFCON 2023, Kocha Erik ten Hag, atalazimika kutoa mechi ya kwanza kwa kipa chaguo la pili, Altay Bayindir.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 hajaichezea United tangu kuhama kwake kutoka Fenerbahce majira ya joto, lakini aliichezea Uturuki wakati wa mapumziko ya mwisho ya kimataifa.

Ten Hag pia ana Tom Heaton mwenye umri wa miaka 37 kwenye kikosi chake.

Hugo Loris kucheza soka MLS
Young Africans yafunguka usajili wa Okrah