Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2024 nchini, usiwe kigezo cha kugawa wananchi bali waungane, wapendane na wathaminiane, ili kuendelea kudumisha amani iliyopo.

Biteko amesema hayo hii leo Januari Mosi, 2024 wakati alipojumuika na wananchi wa Bukombe katika sherehe za kuukaribisha mwaka 2024 nyumbani kwake kitongoji cha Bulangwa, Wilayani Bukombe Mkoani Geita.

Amesema, “mwaka huu utakuwa mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kamwe uchaguzi huu usitugawe kwa misingi ya vyama vya siasa lakini utuunganishe zaidi, watu wote tunapaswa tupendane, tuthaminiane na tushirikiane, tunazo tofauti nyingi  ikiwemo za makabila, dini na vyama vya siasa lakini kamwe visitugawanye, tuungane wote na tushikamane.”

Dkt. Biteko pia amewashukuru wananchi wa Bukombe kwa ushirikiano wanaompa katika utekelezaji wa majukumu yake akisema wamekuwa si watu wa kunung’unika bali kuboresha pale penye mapungufu.

Aidha, katika salamu zake za mwaka mpya 2024, Dkt. Biteko ametaka wananchi kupendana, kuthaminiana na kushirikiana  na kila mtu aazimie kumfanya mtu mmoja awe na furaha na kusameheana.

Sherehe za kukaribisha mwaka 2024 wilayani Bukombe zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, Wabunge  wa Mkoa wa Geita, Madiwani wa Kata mbalimbali wilayani Bukombe na viongozi wa Vijiji.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 2, 2024
Misime awahimiza Wazazi kuwapa malezi bora Watoto