Waumini wa Kanisa la EAGT Kati lililopo kata ya Mlowo Wilayani Mbozi, wametakiwa kuwapa malezi bora watoto wao, ili kutengeneza kizazi bora kwa maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime, aliposhiriki ibada na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa malezi bora kwa watoto na kuwajenga kiimani, ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu na vile vya mmomonyoko wa maadili.

Amesema, “malezi bora kwa watoto yanaanza na maelewano katika ndoa kama mnaishi vizuri bila migogoro kwenye ndoa zenu bila shaka watoto wenu watajifunza tabia njema na watakuwa wazazi wazuri wa watoto wao katika maisha yao ya baadae na tutapata kizazi bora ambacho kinafata mila na desturi za Mtanzania.”

Misime aliongeza kuwa, kumcha Mungu ni kuyatenda yale yote aliyoyaelekeza katika biblia na vitabu vitakatifu pia kuyaishi ikiwa ni pamoja na kuwabariki watoto wetu toka wakiwa wadogo kwa yale mema wayafanyayo ili kutokomeza vitendo viovu katika jamii na hapo tutakuwa tumetengeneza kizazi bora na familia isiyokuwa na mhalifu.

“Nawaomba wazee mliopo kweye ibada hii mkae na wajuuku zenu kama mlivyokuwa mnakaa na sisi kwa lengo la kuwaadithia hadithi za kwenye Biblia na kuwafundisha malezi bora kwa watoto kama kwa lengo la kumjenga mtoto kwenye malezi mema ambayo yatapelekea kuwa na kizazi bora kwa mustakabari wa nchi yetu”. Alisema Misime.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi Theopista Mallya alisema kasi ya utoaji elimu kwa jamii imeongezeka na wananchi wamekuwa wakitoa taarifa za matukio mbalimbali jambo ambalo limesababisha kupungua kwa uhalifu na wahalifu mkoani Songwe.

Naye mchungaji wa kanisa hilo, Alfred Mahenge amelishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu waliyoitoa na ameahidi kuendelea kukemea vitendo viovu kupitia waumini wake ili kupunguza matendo maaovu katika jamii.

Polisi Moro wanasa Lori lililosheheni Bangi, Dereva akimbia

Uchaguzi Serikali za Mitaa usitugawe - Dkt. Biteko
Danadana Treni ya SGR: Rais Samia avunja ukimya