Kocha wa SL Benfica, Roger Schmidt amewaonya Manchester United juu ya mpango wa kwenda kumsajili kiungo kinda, Joao Neves.
Neves mwenye umri wa miaka 19, amekuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu ya Ureno chini ya Schmidt na jambo hilo limemfanya kuwa mmoja kati ya wachezaji wanaowindwa na timu kubwa za Barani Ulaya.
Maskauti wa Man United walitumwa kwenda kumwaangalia mchezaji huyo na kinachoelezwa ni kwamba Kocha Erik ten Hag amevutiwa naye na kumtaka akakipige kwenye kikosi chake.
Licha ya kuwapo na uwezekano wa kutokea kwa usajili mkubwa kumhusu Neves, Benfica inapambana abaki kwenye kikosi chao huku Kocha Schmidt akisisitiza si Neves wala Antonio Silva ambaye pia anawindwa na Man United atakayeruhusiwa kuondoka Januari.
Schmidt alisema: “Nazungumza nao kila siku. Tuna malengo makubwa hapa Benfica na hao ndio tunaotaka wafanye. Hakuna anayetaka kuondoka, sina shaka juu ya hilo.”
Neves inaripotiwa kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachofichua kwamba endapo timu italipa Pauni 105 milioni itanasa saini yake.
Kinda huyo mwenye kipaji amepata nafasi ya kucheza pia kwenye Timu ya Taifa ya Ureno, mahali ambako amekutana na nahodha wa Man United, Bruno Fernandes.
Fernandes alisema: “Ni kocha wa Man United ndiye anayefahamu kama ana nafasi au la. Ni mchezaji mzuri, lakini inategemea na kocha anavyotaka.”