Lydia Mollel – Morogoro.
Wakazi wa Kitongoji cha Yeriko kilichopo Kijiji na Kata ya Kalengakelu, wametakiwa kuwalinda wazee dhidi ya Waganga wakienyeji na wasio waadilifu, wanaowatuhumu kwa uchawi pamoja na watu wanaowafanyia vitendo vya Ukatili.
Hayo yamejiri mara baada ya Bibi Khadija Hassan kutoa malalamiko kuhusiana na usalama wake kwa Polisi Kata wa Kata hiyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Godfrey Nyambala alipokuwa akitoa elimu kwa wakazi hao, Januari Mosi 2024.
Akiongea na Wakazi hao Mkaguzi Nyambala amesema ni lazima watu wote kupitia katika kipindi cha uzee hivyo na je watakuwa tayari kuitwa wachawi.
Amesema, “Watu wote mliokusanyika hapa ni wazee watarajiwa, Je mtakuwa tayari kutengwa na kuitwa wachawi pindi mtakapofika miaka 60?Ni jukumu la kila mwanajamii kumlinda kikongwe aliepo maeneo yake bila kujali ni ndugu au sio ndugu yake.”
Aidha, Nyambala pia amewataka wananchi hao kujiunga na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi,kutoa taarifa sahihi za Uhalifu na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya Ukatili wa Kijinsia wa Wazee na watoto ili kuufanya mwaka huu 2024 kuwa salama na amani kwao.