Lydia Mollel – Morogoro.
Dhana ya kuhofia kuwa karibu na Jeshi la Polisi iliyojengeka kwa Vijana wengi nchini imetakiwa kuondoka, ili kujenga ushirikiano wa pamoja katika kuzuia na kutokomeza Uhalifu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Malinyi, Samweli Kijangwa katika bonanza la mpira wa miguu liloandaliwa na Jeshi la Polisi kwa lengo la kuwaweka Vijana karibu na Jeshi hilo, ili kuifanya Wilaya hiyo kuwa salaama kwa kipindi chote cha 2024.
Amewataka wachezaji na vijana waliokusanyika uwanjani hapo kutumia michezo hiyo kuleta amani na kuachana na vitendo vya uhalifu huku akiwahimiza kujiunga kwenye vikundi vya Ulinzi Shirikishi ili kuzuia na kupambana na uhalifu.
Aidha OCD Kijangwa pia amewataka kujenga mahusiano na ushirikishwaji jamii kwa kupata taarifa mbalimbali za vitendo vya uhalifu , lakini pia kuondokana na matendo hasi yanayochangia kufanya vitendo vya uhalifu na vurugu mfano kutojihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya,unywaji wa pombe kupitiliza,ukabaji na wizi.
Katika bonanza hilo OCD Kijangwa alikabidhi Tsh 500,000/= kwa Masofa Fc washindi wa Mashindano hayo, Tsh. 300,000/= kwa Igawa Fc ambao ni washindi pili na Tsh 200,000/= kwa Nawigo Academy ambao walishika nafasi ya tatu.
Nahodha wa timu ya Masofa Fc Rahisi Mnape, amesema wao kama wachezaji wamefurahishwa na wazo hilo la kuwaunganisha pamoja kupitia michezo lakini pia ameahidi kuufanyia kazi ujumbe uliotolewa kwa kuanza kushirikiana na Jeshi la Polisi kuilinda Malinyi.
Kwa upande wake, Mzee Saidi Kachwela aliekuja kushuhudia bonanza hilo, alimpongeza OCD na Askari kwa ujumla kutokana na njia waliyotumia kuunza mwaka kwani itawafanya wananchi kujenga imani na Jeshi la Polisi na kutoa ushirikiano.
Endapo jamii itashirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za awali pindi wanapokuwa na mashaka na jambo au kutoa taarifa zozote za kihualifu ni wazi kuwa itasaidia Jeshi hilo kubaini vitendo vyote vya kiuhalifu vinavyoendelea katika jamii zetu na kuimarisha ulinzi na usalama.