Kikosi cha Coastal Union kinatarajia kuingia kambini kesho Jumamosi (Januari 06) kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Mashindano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Msemaji wa timu hiyo, Abbas El-Sabri amesema walitoa mapumziko ya majuma mawili kwa wachezaji wao kwa ajili ya sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya na baada ya kumalizika wanarudi kambini kujiweka sawa ili kutimiza malengo waliyojiwekea msimu huu 2023/24.
El Sabri amesema pamoja na hayo pia wamekusudia kuongeza wachezaji wanne kwenye dirisha hili dogo la usajili ambapo wawili kati yao ni raia wa Kenya na wapo katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za usajili.
Amesema mpaka sasa wameshakamilisha usajili wa wachezaji wawili ambao ni Salim Ayee pamoja na Fiston Abdulrazak kutoka Gor Mahia ya Kenya.
Kiongozi huyo amesema lengo lao kubwa msimu huu ni kuhakikisha wanamaliza msimu kwenye nafasi nne za juu na kufika fainali kwenye Kombe la ‘ASFC’.
Coastal Union inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 19 katika michezo 14 iliyocheza hadi sasa, huku wakibakiza mchezo mmoja kukamilisha mzunguko wa kwanza.