Mlinda Lango Andre Onana anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Man Utd kitakachopambana na Tottenham Hotspur katika mchezo wa Ligi Kuu ya England, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa na Shirikisho la Soka nchini kwake Cameroon.

Makubaliano hayo yatamfanya Onana kuchelewa sehemu ya Maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, zinazotarajiwa kuanza nchini Ivory Coast, Januari 13.

Onana amepewa ruhusa ya kusalia Manchester kwa mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Wigan Athletic itakayochezwa Jumatatu watakapoikaribisha Spurs kwenye Uwanja wa Old Trafford Januari 14, mwaka huu.

Klabu za Ligi Kuu England zilipewa muda hadi Januari Mosi kuwaachia wachezaji wao kabla ya michuano hiyo itakayofanyika Ivory Coast kuanzia Januari 13, Mwaka huu lakini United na Cameroon wamekubaliana kumchelewesha Onana.

Onana alirejea Manchester juzi baada ya kukaa kwa muda jijini Paris kufuatia kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Nottingham Forest Jumamosi ililyopita.

Kikosi cha Cameroon kwa sasa kinaendelea na mazoezi katika kambi yake iliyoko Saudi Arabia, ambapo wanatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia Januari 9, mwaka huu.

Onana, ameonyesha nia ya kupunguza muda wake nje ya United baada ya kuiambia klabu hiyo wakati wa mazungumzo ya uhamisho wa majira yajoto amestaafu soka la kimataifa.

Kipa huyo aliachwa wakati wa Fainali za Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, kufuatia kutofautiana na Kocha, Rigobert Song, lakini akashawishiwa kurejea kabla ya mechi ya mwisho ya kufuzu AFCON 2023 dhidi ya Burundi mwezi Septemba, mwaka jana.

Kinda la Kibrazil tishio FC Barcelona
Gwiji wa soka Algeria atabiri mazito AFCON 2023