Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ wa mpira, Jadon Sancho ameripotiwa bado hajakata tamaa maisha yake ya kuitumikia Manchester United ndiyo yamefika ukomo, akiamini atarejea Old Trafford mwishoni mwa msimu huu.
Staa huyo wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 23, hajaichezea Man United tangu mwishoni kwa Agosti mwaka jana baada ya kutibuana na kocha Erik ten Hag kufuatia kumuweka benchi kwenye mechi ya Arsenal mwanzoni mwa Septemba.
Ten Hag alisema alimwondoa Sancho kwenye kikosi chake cha mechi hiyo ya Arsenal kwa kuwa hakufanya vizuri mazoezini, kitu ambacho staa huyo wa zamani wa Manchester City na Borussia Dortmund alijibu si kweli na kinachofanyika ni kumgeuza tu kuwa mbuzi wa kafara.
Tangu hapo, Ten Hag na Sancho uhusiano wao ukaingia dosari na hivyo kushindwa kuitumikia Man United.
Katika dirisha hili la uhamisho wa Januari taarifa zinaeleza kuwa, Sancho yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wake wa mkopo wa kurudi tena Borussia Dortmund hadi mwishoni mwa msimu.
Awali, ilidhaniwa Dortmund itakuwa na ruhusa ya kumchukua jumla staa huyo mwishoni mwa msimu, lakini ripoti mpya zinafichua hakuna kipengele kama hicho, hivyo Sancho atarejea Old Trafford baada ya msimu huu.
Hilo limewekwa baada ya kuona kocha Ten Hag yupo kwenye presha kubwa sasa kutokana na timu yake kufanya ovyo na hadi sasa imeshakumbana na vichapo 14 ndani ya msimu huu, kama atashindwa kuvuna matokeo mazuri kwenye mzunguko wa pili wa msimu, bila ya shaka ataonyeshwa mlango wa kutokea na hapo Sancho atarudi Old Trafford kukutana na kocha mpya.
Kwenye dili la Dortmund, miamba hiyo ya Bundesliga imekubali kulipa mshahara wa Sancho kati ya asilimia 30 na 40, hivyo kuwafanya Man United iendelee kulipa sehemu kubwa iliyobaki hadi mwisho wa msimu.