Uongozi wa Tanzania Prisons umefichua kuwa kocha wao, Ahmad Ally kwenye dirisha hili dogo la usajili linaloendelea anataka kuongeza wachezaji kwenye nafasi tatu pekee katika kikosi hicho.
Uongozi huo umeyataja maeneo ya ushambuliaji, kiungo na beki mmoja ndiyo nafasi ambazo kocha huyo anazitaka na wao wamekuwa wakifanya usajili wao kimyakimya kwa kuzingatia ripoti ya kocha huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Prisons, Ajabu Kifukwe amesema kuwa kwa sasa kinachoendelea kwao ni usajili katika kipindi hiki cha mapumziko.
“Kikosi kinaendelea vizuri, ligi imesimama tupo katika hatua za kuifanyia kazi ripoti ya mwalimu kwa utulivu katika kipindi hiki cha mapumziko na dirisha dogo. Ripoti inahitaji kuboresha katika maeneo ya ushambuliaji, kiungo na ulinzi.
“Uongozi na benchi la ufundi tunashirikiana vyema kuhakikisha tunapata wachezaji wazuri watakaoingia katika kikosi moja kwa moja na kuanza kutatua changamoto zilizopo katika kikosi chetu, kwa sababu dirisha dogo ni kwa ajili ya kusajili mchezaji anayeingia kikosini na siyo kumpa mechi za kutazama.
“Siyo kwamba tuna wachezaji wabovu, tunao wachezaji wazuri wenye uwezo wa kupambana, tunachofanya ni kuboresha tulichonacho, tunategemea kusajili wachezaji wanne na tayari tumeshawapata wachezaji wawili, bado tunashughulikia wawili kukamilisha dirisha hili dogo,” amesema Kifukwe.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya ligi kusimama, Prisons walikuwa wamejizolea pointi 17 baada ya kucheza mechi 14 wakiwa katika nafasi ya tisa 9.