Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Adel Amrouche anaamini michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ ni tukio muhimu zaidi Barani Afrika na wachezaji wake wamejandaa kulichukulia hivyo.
Amrouche amesema hayo baada ya kuwasili Ivory Coast na kikosi cha Taifa Stars akitokea Cairo, Misri walipoweka kambi na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri ambapo walifungwa mabao 2-0.
Amesema wachezaji wake wana hamu ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.
“Wachezaji wanajua haya ni mashindano makubwa na ni tukio kubwa zaidi Barani Afrika. Itawapa fursa kubwa wanapocheza dhidi ya mataifa maarufu katika soka. Ni tukio kubwa zaidi na ni ndoto nzuri ya kucheza ‘AFCON 2023’. Nina furaha kwani wachezaji hawa wanastahili,” amesema.
Taifa Stars itaanza kampeni zake kwenye michuano hiyo kwa kuikabili Morocco Januari 17 kabla ya kuivaa Zambia siku nne baadae na watamaliza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Januari 24.
Katika hatua nyingine Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amewataka wadau wa sekta mbalimbali kuzisaidia timu za taifa kwani sio rahisi kwa serikali pekee kuzihudumia timu zote.
Ndumbaro amesema hayo wakati wa uzinduzi wa harambee wa kuzichangia Taifa Stars na timu ya soka ya taifa ya wanawake ambazo zote zitashiriki fainali za mataifa ya Afrika mwaka huu lvory Coast na Morocco.