Baada ya kuhusishwa kujiunga na Young Africans, winga wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Simon Msuva kwa mara ya kwanza tangu aachane na timu ya JS Kabylie ya Algeria amesema kuwa lolote linaweza kutokea akacheza ligi ya ndani au nje ya nchi.

Msuva ambaye aliachana na timu hiyo mwishoni mwa mwaka jana baada ya kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa kutoka kwake, kwa sasa yupo na Stars akijiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’.

Hata hivyo alipomtafuta Msuva ili kuzungumzia mustakabali baada ya taarifa kuzagaa kuwa anatarajiwa kujiunga na Young Africans, alijibu kuwa hakuna linaloshindikana kwenye soka.

“Nina ofa japo nyingine ni tetesi zinazungumzwa tu kutokana na kubaini mimi ni mchezaji huru.

Ninachoweza kusema kwa sasa tusubiri mambo yakamilike kila mmoja atafahamu nitacheza wapi, lakini jambo la msingi ni kwamba chochote kinaweza kutokea,” amesema Msuva.

“Kucheza Tanzania au nje ya Tanzania lolote linawezekana tusubiri muda utazungumza. Sitaki kuwa mzungumzaji kwa sasa napambana kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri kwenye fainali za AFCON 2023.”

Msuva alifanikiwa kuzitumikia timu kubwa ikiwemo Wydad Casablanca na Difaa El Jadida za nchini Morocco.

CCM chatoa maoni, ushauri Miswada minne ya Sheria
Nice yamng'ang'ania Jean-Clair Todibo