Klabu ya Dodoma Jiji imekamilisha usajili wa nyota wawili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kuongeza nguvu katika dirisha hili dogo la usajili linalofungwa rasmi leo Jumatatu (Januari 15) ikiwa ni mapendekezo ya kocha mkuu wa kikosi hicho Mkenya, Francis Baraza.
Wachezaji waliosajiliwaa na kikosi hicho ni beki wa kati, Robinson Kamura aliyetoka klabu ya Kakamega Homeboyz na kiungo mshambuliaji, Apollo Otieno kutoka KCB ambao wote kwa pamoja wamepewa mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu hiyo.
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza alisema hawezi kuthibitisha juu ya usajili huo hadi pale viongozi watakapoweka wazi kwani yeye tayari alishapendekeza wachezaji anaowahitaji ili kuongeza nguvu kikosini.
“Kazi iliyobaki ni kwa viongozi kukamilisha mahitaji niliyowapa na naamini maendeleo ni mazuri hadi sasa, hivyo ni suala la kusubiri kwa sababu usajili unafungwa leo na kila kitu tutaweka wazi kwa walioingia na wale tutakaowaacha,” amesema.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Patrick Semindu amesema bado wanaendelea kupambana na baadhi ya wachezaji wanaowahitaji na hadi kufikia leo anaamini kwa kiasi kikubwa watafanikiwa kwa wale wote wanaowataka.
Mbali na usajili huo wa kigeni, kikosi hicho kiko mbioni kukamilisha dili la Denis Nkane.