Viongozi wa Serikali za Kenya na Tanzania wamesema wanafanya juhudi kuutatua mvutano ulioibuka, kufuatia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini – TCAA kutangaza kufuta kibali cha safari za ndege za shirika la Kenya Airways kati ya Nairobi na Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya TCAA, ilikuwa ni ya kujibu msimamo wa Serikali ya Kenya ya kukataa kutoa kibali cha kuingia Kenya kwa ndege za mizigo za kampuni ya ndege ya Air Tanzania.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya, Musalia Mudavadi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Januari Makamba wamesema wamefanya mawasiliano kwa njia ya simu na kukubaliana kuutafutia ufumbuzi mvutano uliojitokeza.
Makamba amesema, “vizuizi vya usafiri wa anga kati ya nchi zetu na kutoka miongoni mwa nchi hizo kwenda nchi nyingine haupaswi kuwepo,” huku Mudavadi naye akisema “hakuna sababu ya kuwepo wasiwasi kwa sababu tayari tumekubaliana kuwa mamlaka za usafiri wa anga za pande zote zitatatua mvutano uliojitokeza.”