Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP), unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia umeongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini kutoka asilimia 25 hadi 35, hatua inayosaidia kuinua kiuchumi wao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mradi LTIP, Joseph Shewiyo unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati akifungua kikao kazi cha Asasi za kiraia kujadili utekelezaji wa mradi huo Januari 16, 2024 jijini Dodoma.
Amesema, “mna jukumu kubwa, mnapaswa kuongeza wigo katika kutekeleza majukumu yenu kufanikisha kutoa hati milki za kimila ili kuinua uchumi wa wananchi, mna mchango mkubwa kwa ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 25 hadi 35, mkafanye kazi yenu kwa weledi msiharibu ndoa za watu.”
Mradi huo, unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia unalenga kuimarisha mifumo ya utawala wa ardhi, kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa wanaume na wanawake na hivyo kukuza uwekezaji wa ardhi nchini.
Majukumu yanayotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa kupanga, kupima na kumilikisha wananchi ardhi mijini na vijijini, kuboresha mifumo ya usimamizi wa taarifa za ardhi nchini, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mradi.