Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Jumatano (Januari 17) itakuwa na kazi moja tu kwenye Uwanja wa San Pedro nchini Ivory Coast, kujaribu kuweka rekodi ya kushinda kwa mara ya kwanza katika mechi ya makundi ya Mataifa ya Afrika (AFCON), itakapocheza dhidi ya Morocco saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku Kocha Mkuu Mkuu, Adel Amrouche, akisema amewaandaa vema wachezaji wake kwa ajili ya mechi hiyo.

Stars haijawahi kushinda mechi yoyote ya fainali za AFCON mara zote mbili ambazo imefanikiwa kuingia mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 nchini Misri.

Amrouche amesema wachezaji wake wako fiti kwa asilimia 99 na amewataka kuweka rekodi nzuri kwenye michuano hii zaidi ya iliyopita.

“Ni mechi ngumu, Morocco ni moja kati ya timu vigogo vya soka barani Afrika, lakini tumeona katika michuano hii timu zile zinazoonekana ndogo zikizifunga au kuwasimamisha vigogo, hivyo hakuna chochote ambacho tutahofia kucheza na timu hiyo kwa nia moja tu ya kupata ushindi,” amesema kocha huyo.

Amesema anachosubiri ni muda ufike ili wachezaji wake wakakitoe kile ambacho amekuwa akiwafundisha katika uwanja wa mazoezi.

Naye Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro ambaye yupo nchini humo kwa ajili ya kuisapoti Stars, amesema baada ya kuitembelea kambi pamoja na mazoezi ya mwisho alichokiona ni morali ya hali ya juu kwa wachezaji.

“Nimepata fursa ya kumsalimia kila mchezaji na kila aliyekuwapo kwenye benchi la ufundi, nilichokiona timu ipo timamu, morali ipa juu sana, hii inanipa moyo kwamba timu yetu sasa ipo tayari kupambana kwenye mashindano haya, mtaalam wa viungo ameniambia wachezaji wako fiti kuikabill Morocco na hata Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,” amesema Dk Ndumbalo.

Naye Rais wa Shirikisho la Soka ‘TFF’, Wallace Karia, amewatoa wasiwasi Watanzania kuhusu hali ya hewa ya huko akisema haitowaathiri sana wachezaji kwa sababu ni kama ya Dar es salaam tu, huku akiongeza kuwa wapo kwa ajili ya kuipa sapoti Stars, lakini pia kujifunza kwa sababu 2027, Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Stars ambayo ipo Kundi F, itacheza mechi hiyo saa mbili usiku, huku Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambazo nazo zipo kwenye kundi hilo, zikitarajiwa kucheza saa 5:00 usiku.

Mwaka 1980 ikiwa Kundi A, Stars ilimaliza mechi zake za AFCON ikiwa imecheza mechi tatu, ikipoteza mbili na sare moja ikishika nafasi ya mwisho, na 2019 ilipotinga kwa mara ya pili ilimaliza ikiwa imepoteza mechi zote tatu ikishika nafasi ya mwisho katika Kundi C.

Idadi Wanawake wanaomiliki ardhi Nchini yaongezeka
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Januari 17, 2024