Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha huduma za afya ngazi zote na imekamilisha ujenzi wa Hospitali za Wilaya na itajenga Hospitali mpya kwa kila mkoa Zanzibar.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipofungua jengo jipya la huduma za matibabu ya dharura na maabara ya kisasa katika kituo cha afya Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja hii leo Januari 17, 2024.
Amesema, mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya msingi kwa kujenga majengo mapya, kuweka vifaa vya kisasa kwa lengo la kutoa huduma za uchunguzi na dharura.
Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa, Serikali imelenga kuzisogeza huduma zote muhimu za afya kuwa karibu na wananchi ikiwa pamoja na kuweka mifumo ya tehama, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili kurahisisha huduma za matibabu na uchunguzi kwa wakati wote.