Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.

Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia za Tanzania zaidi ya shilingi milioni 13, 550,000 pamoja na mtambo wa kutengeneza pesa bandia.

Kamanda wa Polisi Kkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo amesema tukio hilo limetokea Januari 10, 2024  katika Kijiji cha Msata kilichopo Wilaya ya Kipolisi Chalinze na kuwataja watu hao kuwa ni pamoja na Mbaraka Miraji Fundi (48), na Zena Issa Naringa (42), wote wakazi wa Buza jijini Dar es Salaam.

Amesema, jukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na taarifa za raia mwema aliyeitilia mashaka noti ya Sh. 10,000 aliyoipokea kama malipo ya huduma katika nyumba ya kulala wageni huko Msata.

“Baada ya mahojiano na watuhumiwa, Polisi walifanikiwa kuwabaini washirika wao ambao ni Masumbuko Paul Kiyogoma (54), mkazi wa Goba na Elias Silas Wandiba (50), mkazi wa Kimara Suka wote wa jijini Dar es salaam wakiwa na pesa nyingine bandia zenye thamani ya shilingi 12,000,000 za noti za 10000, 5000 na 2000,” alisema.

Aidha katika upekuezi kwenye makazi yao Polisi walifanikiwa kukamata mtambo wa kutengeneza pesa hizo bandia na zana zingine kama vile computa, kemikali mbalimbali, gundi jiki, tina, rangi, visu na bunda la karatasi zikiwa katika hatua mbalimbali za kutengenezwa fedha bandia.

“Mtambo huo wa kutengeneza pesa bandia ulikamatwa katika makazi ya mmoja wa watuhumiwa huko Goba jijini Dar es salaam” alisema Kamanda Lutumo.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa taadhali kwa wanannchi kuwa makini na fedha wanazopokea kutoka kwa watu wasiowafahamu ikiwa ni pamoja na wateja wao kwa kuzikagua na kuhakiki alama za fedha halali zinazokuwepo.

Makamba, Mudavadi wajadili changamoto ustawi wa Biashara
Usajili Dirisha Dogo wamchizisha Kiongozi Simba SC