Diwani wa Kata ya Lukobe Mkoani Morogoro, Selestine Mbilinyi ameiomba Serikali kuwatengenezea miundo mbinu itakayosaidia kupitisha maji na kupeleka mto Ngerengere, ili kuepusha usambaaji wake kwenye makazi ya watu.
Hayo, yamejiri kufuatia Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Morogoro na kusababisha baadhi ya Nyumba kubomoka, kuharibu miundombinu ya Barabara na kusababisha shughuli za kibinadamu kukwama.
Aidha, chanzo cha uharibifu huo kinatajwa kuwa ni ujenzi wa Daraja la Mwendokasi katika kata hiyo kwani matuta yaliyopo yamezuia mkondo wa maji na kupelekea yatafute njia kuja kwenye makazi ya Wananchi.
Licha ya Serikali kufanya utafiti na kugundua changamoto hiyo, bado jitihada ya kutatua haijafanyika hivyo Mbilinyi ameiomba kulifanyia kazi jambo hilo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.