Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema utajiri wa nchi na kupiga hatua kimaendeleo kwa haraka hakutokani na ukubwa wa nchi bali ni maono sahihi ya viongozi bora, wanaoweza kusimamia kwa ujasiria na uadilifu sera na rasilimali zilizopo.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo Mkoani Lindi wakati alipokuwa akizungunza na Viongozi wa chama kwenye ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa ACT- Wazalendo ngazi ya Mikoa, unaondelea nchini kote.
Amesema, maono bora ya viongozi ni utajiri mkubwa kuliko chochote ndani ya nchi kwani yapo mataifa kadhaa yaliyoweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo, licha ya kuwa na rasilimali chache kuliko zile zilizopo Tanzania.
Aidha Othman pia ameongeza kuwa, jambo kuwa uwepo maono, uadilifu na uaminifu na ujasiri wa viongozi sambamba na uwajibikaji bora wa watendaji wenye dhamana waliopo katika ngazi mbali mbali, utasaidia kubadilisha maisha ya Wananchi na Taifa zima kwa ujumla.