Bertina Mangosongo.
Takriban Watu 573 wamepatiwa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu ijulikanayo kwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora –KITETE.
Kambi hiyo iliyofanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 15 Januari imemalizika tarehe 19 Januari 2024 mkoani Tabora ambapo jumla ya watu wazima 531 na watoto 42 walipatiwa matibabu.
Akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa wa Tabora kuhusu kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Parvina Kazahura alisema wametoa rufaa kwa wagonjwa 84 wakiwemo watoto na watu wazima kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwani wanahitaji kupatiwa matibabu zaidi.
Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda Buriani amewashukuru wataalamu wa afya wa JKCI na kuwaomba kufikisha salamu kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo kwa kuwafikishia huduma za matibabu ya moyo huku akiomba huduma ya tiba mkoba mkoani Tabora isiishie hapo, bali Taasisi ya Moyo ijipange kurejea tena mkoani humo kwani bado wananchi wa Tabora wanawahitaji sana.