Bertina Mangosongo – Dar es Salaam.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, kinaendelea na maandamano kupinga mapendekezo ya miswada ya sheria ya Uchaguzi, gharama kubwa ya maisha na kucheleweshwa kwa marekebisho ya Katiba, ambapo viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Makamu Tundu Lissu wameshiriki.

Mandamano hayo yanafanyika kwa amani na Polisi waliridhia yafanyike katika jiji la Dar es Salaam, ingawa walionya juu ya vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwemo ghasia na uchochezi.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema maandamano hayo yanalenga kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali, kuhusu masuala ya uchaguzi.

Alisema, wanaitaka serikali iondoe Bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi, ambayo ni muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa na Sheria ya gharama za Uchaguzi.

Aidha, Mbowe aliongeza kuwa Serikali inatakiwa wasilishe muswada wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia mwafaka wa kitaifa. Kwani wanaamini imepuuza maoni yaliyotolewa na Kikosi kazi pamoja na wadau mbalimbali.

Hata hivyo, CHADEMA pia wanaitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na ule mkuu wa 2025 uwe huru na haki.

Zifuatazo ni baadhi ya picha ambazo zinaonesha matukio mbalimbali wakati wa maandamano hayo.

 

 

Kocha JKT afurahia usajili wa Kichuya
Azam FC yapeleka salamu Ligi Kuu