Kuelekea kilele cha wiki ya Sheria itakayoazimishwa maeneo mbalimbali nchini, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzifahamu haki zao na namna ya kuzifuatilia.
Akitoa elimu kwa wakazi wa Kijiji cha Luhombero Kata ya Ilonga Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Kelvin Makaranga amesema, kila mwananchi anaruhusiwa kumuwekea dhamana ndungu yake anayeshikiliwa kwa makosa mbalimbali kwenye vituo vya Polisi bila ya kutoa pesa.
Awali akizungumza na wakazi hao, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Paulina Aidan ambaye ni Polisi wa Kata hiyo amesema, mbali na dhamana bure pia wanapaswa kuzijua haki zao na kuzifuatilia badala ya kudai wanaonewa au kudhulumiwa na taasisi za watu wengine.
Aidha, Mkaguzi Aidan pia aliwafundisha juu ya miradi ya Polisi Jamii ikiwemo, Usalama wetu kwanza, familia yangu haina muhalifu na kutii sheria bila shuruti.