Dawa za kulevya aina ya amphetamine methamphetamine na mirungi, zimetajwa kuwa ni hatari kwa afya ya mtumiaji, kwani huathiri utendaji wa mfumo wa fahamu, husababisha kukosa usingizi, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kiharusi na vifo vya ghafla.

Hayo yamebainishwa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, Aretas Lyimo na kuongeza kuwa pia dawa za kulevya aina ya cocaine huweza kusababisha matatizo ya afya ya akili na husababisha hasira, ukatili, vurugu, kukosa utulivu na hata mtumiaji kutaka kujiua.

Amesema, “Dawa hii husababisha uraibu wa haraka na utegemezi na hivyo, kuwa vigumu kwa mtumiaji kuiacha. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itafanya operesheni kali za nchi kavu na baharini kwa mwaka huu 2024.”

Aidha, Kamishna Lyimo amebainisha kuwa, zitafanyika operasheni za nchi kavu zitakazohusisha mashamba ya dawa za kulevya, kwenye mipaka, maeneo ya mijini kwenye vijiwe vya usambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya na kusema upande na baharini, zitahusisha fukwe na katikati ya bahari.

Operasheni hizo, zitahusisha maeneo yote wanayouza shisha ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ambapo wale wote watakaobainika kutumia dawa za kulevya kupitia shisha watachukuliwa hatua kali za kisheria. Vilevile, operasheni hii itahusisha wauzaji
wanaokiuka taratibu za uuzaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu.

Amesema, Mamlaka inatoa onyo kwa wote watakaoendelea kujihusisha na uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha kwani, Serikali imeendelea kuiwezesha Mamlaka kwa kununua vifaa vya kisasa na mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka na hivyo kuwajengea ujasiri na weledi katika kutekeleza operasheni kwa ufanisi mkubwa.

Hivyo, kwa wale wote watakaoendelea na kilimo cha bangi, mirungi na biashara ya dawa za kulevya za viwandani watashughuliwa na kwamba Mamlaka inawaomba wananchi kuendelea kutoa kutoa taarifa za watu wote wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya.

Mashabiki Young Africans waahidiwa furaha
AFCON 2023 yamng’oa Djamel Belmadi