Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema katika jitihada za kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu Nchini watatumia mashindano yajayo ya Bunge Marathon kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum ya wavulana.
Dkt. Tulia ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akihitimisha mashindano ya Azania Bunge Bonanza yaliyoandaliwa na Benki ya Azania ambapo amesema kuwa tayari bunge limeshajenga shule maalum ya wasichana iliyopo eneo la Kikombo Jijini Dodoma na walijenga kwa kutumia pesa za mashindano ya riadha.
“Mashindano ya riadha yajayo yatatumika kukusanya fedha kwa ajili ya kujenga shule maalum ya wavulana hivyo tutangaza wapi shule hiyo itajengwa,hii ni kutokana na kuwa bunge letu lina wanaume hivyo tutajenga pia shule ili tuwe na shule mbili ya wasichana na wavulana”,amesema
Hata hivyo, Spika Tulia ameipongeza Benki ya Azania kwa kuandaa bonanza hilo kwa wabunge na pia amewashukuru washindi waliopatikana katika mashindano hayo.
“Napongeza tamasha la michezo kwa Wabunge,Watumishi pamoja na hamasa kubwa iliyofanywa na Yanga SC chini ya Afisa habari wetu Ali Kamwe”. Amesema Dkt.Tulia
Mashindano ya Azania Bunge Bonanza yamedhaminiwa na Azania Bank ambapo yamewakutanisha mashabiki wa timu ya Simba na Yanga ikiwa ni Wabunge na wafanyakazi wa bunge.
Katika Mpira wa Miguu timu ya wabunge wa Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya wabunge wa Simba SC kwa Mikwaju ya Penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa kufungana bao 1-1.