Waziri wa Vijana na Michezo wa Misri Ashraf Sobhy ametoa maoni yake kuhusu mustakabali wa Kocha Mkuu wa sasa wa Timu ya Taifa ya nchi hiyo Rui Vitoria, huku akithibitisha uwezekano wa kurejeshwa kwa Kocha kutoka nchini Ureno Carlos Queiroz.
Misri ilitupwa nje ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ baada ya kushindwa na DR Congo kwa Mikwaju ya Penati na kumaliza ndoto zao za kutawazwa kuwa mabingwa wa bara hilo mwaka huu.
Mafarao walifuzu kwa hatua ya mtoano baada ya sare ya 2-2 katika Kundi B dhidi ya Msumbiji, Ghana, na Cape Verde mtawalia, kabla ya kuambulia sare nyingine dhidi ya DR Congo.
Kwa ujumla, Kikosi cha Misri kinachonolewa na Kocha Rui Vitoria hakikuweza kushinda mchezo hata mmoja nchini Ivory Coast na walirejea Misri wakiwa na sare nne, jambo ambalo linatia shaka mustakabali wa kocha huyo.
Waziri wa Vijana na Michezo Sobhy amesema: “Mchezo wa Soka unachukua mambo mengi kwa jumla ambayo yanapaswa kufanyiwa maamuzi kwa umakini, na ikibidi kukidhi maono yetu kama watu, lazima tuchunguze na kuelewa sababu.
“Misri iliondoka kwenye Kombe la Dunia la 2018 kwa huzuni, na ilikuwa ni lazima kutathmini upya hali hiyo haraka. Mnamo 2019, tuliandaa AFCON katika ardhi yetu, na timu haikukidhi fahari yetu. Kulikuwa na tathmini ya hali hiyo.
“Katika AFCON ya 2019, Carlos Queiroz alikuja ndani ya miezi sita na kufanikiwa kurekebisha sura ya jumla, na kuiongoza timu hadi fainali. Tuliishauri EFA kwamba kocha huyu asiondoke, lakini uamuzi ukatolewa.
“Kutakuwa na uchaguzi ndani ya EFA ambao utafanyika baada ya Michezo ya Olimpiki mwezi Julai na yeyote aliye na wasifu mzuri ajitokeze. Lakini kutupilia mbali EFA hivi sasa kutatupeleka kwenye mtafaruku usioepukika.
“Mwaka 2024, kuna mechi za kufuzu Kombe la Dunia, na mwaka ujao, 2025, kutakuwa na AFCON huko Morocco. Maandalizi lazima yawe mazuri sana, na EFA ijayo itachukua usukani mwishoni mwa 2024.
“Kwa maoni yangu binafsi, tulikuwa na uzoefu mmoja wa mafanikio na kocha wa ndani, Hassan Shehata, na kabla yake, Mahmoud El-Gohary, ambaye alikuwa kocha wa kipekee. Hata hivyo, hivi karibuni tulijaribu kuwa na Hossam El-Badry na Ehab Gamal, lakini haikufanyiwa kazi. Kwa hivyo, sidhani kama kutakuwa na kocha wa ndani.
“Maoni ya umma ambayo hayana imani na Rui Vitoria yanaheshimiwa kwa sababu maadamu kuna maafikiano, ni maoni halali. Tunaunga mkono hili, lakini lazima tutoe nafasi ya kusikia uhalali wa kocha na aina ya mkataba kati ya EFA na kocha. Lakini hii inapaswa kufanywa haraka.”
Alipoulizwa kama Queiroz anaweza kurejea kuchukua mikoba ya Misri, amesema: “Uwezekano wote uko wazi, lakini lazima kuwe na wataalam. Imani yangu ni kwamba Queiroz, katika kipindi cha miezi sita, aliweza kubadilisha fomu ya timu na kufika fainali ya AFCON 2021.
“Nilisema wakati huo Queiroz aendelee, lakini EFA ilisitisha mkataba wake na kuleta mpya. Timu ya sasa ya makocha haijawasilisha lolote la kuridhisha, hivyo lazima kuwe na uwajibikaji kutoka EFA, na sisi kama wizara tutaweka mazingira yanayofaa kwa timu zote za taifa.”