Kufuatia ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Morocco katika hatua ya 16 Bora ya Fainali za Mataifa ya Afrika zinazoendelea nchini Ivory Coast, Kocha Mkuu wa Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ Hugo Broos amefichua mipango na mikakati ya kikosi chake kuelekea mchezo wa Robo Fainali.
Afrika Kusini itacheza dhidi ya Cape Verde Jumamosi (Februali 03) mjini Yamoussokro, mchezo ambao unatarajiwa kuwa na vuta ni kuvute kutokana na timu hizo kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa kisoka.
Kocha Broos amesema: “Tulikuja hapa tukiwa na lengo la kwanza la kutoka kwenye kundi letu,”
“Tulifurahi kufanya hivyo lakini huwezi kuwa na uhakika wa kwenda mbele zaidi utakapomenyana na Morocco.
“Jumamosi kwa mara nyingine tena tutacheza dhidi ya timu hatari na hatuwezi kufanya makosa ya kuwadharau,” amesema kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji
Wakati Morocco, waliofuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022, wanaongeza orodha inayokua ya wachezaji wenye majina makubwa zaidi barani humo waliotupwa nje katika Fainali za ‘AFCON 2023’, saa 24 baada ya mabingwa Senegal kuondolewa kwa mikwaju ya Penati na wenyeji Ivory Coast.
Kikosi cha Morocco kilikuwa na matumaini ya kufuatia mchujo wao wa kutinga hatua ya nne bora nchini Qatar mwaka mmoja uliopita kwa kushinda taji lao la pili la AFCON, miaka 48 baada ya taji lao la kwanza.
Badala yake wanaenda sawa na Senegal, Tunisia, Algeria na Misri kwa kutupwa nje katika Fainali za ‘AFCON 2023’, ikimaanisha kwamba hakuna taifa hata moja kati ya mataifa matano yaliyo kwenye nafasi ya juu Barani Afrika kisoka, litakalokuwepo kwenye Robo Fainali, na pia hakuna hata mmoja kati ya wanne watakaofuzu Nusu Fainali.
“Tumesikitishwa sana kwa sababu tulikuja hapa tukiwa na nia ya kushinda,” alikiri kocha wa Morocco Walid Regragui.
“Kutoka mapema sana haikuwa katika mipango yetu lakini mashindano haya ni magumu sana.
“Ninawajibika kwa kila kitu kilichotokea. Sifichi kamwe. Leo nimeshindwa,” aliongeza.