Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema katika kuhakikisha Wananchi wa Kata ya Masaki Wilayani Kisarawe wanapata huduma ya majisafi na salama, Serikali kupitia DAWASA imekamilisha usanifu wa kina wa mradi wa maji Kisarawe.
Mhandisi Mahundi ameyasema hayo leo hii leo Januari 31, 2024 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Hawa Mchafu aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa kata ya Masaki – Kisarawe wanapata huduma ya maji safi na salama.
Akijibu swali hilo, Mhandisi Mahundi amesema Mradi huo unatarajia kutekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/25 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 24 na ujenzi wake unatarajia kuchukua Miezi 18.
“Kazi zinazotarajiwa kufanyika kwenye mradi huo ni pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 230, ujenzi wa Tenki 1 lenye ujazo wa lita 1,000,000 na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji chenye tanki la lita 540,000 kitakachofungwa pampu mbili,” amesema Mahundi.
Aidha, Mahundi amesema mradi huo ukikamilika utahudumia Kata tano (5) za Masaki, Msimbu, Kibuta, Kazimzimbwi na Marumbo.