Baadhi ya Wananchi walioathiriwa na mafuriko ya maporomoko ya mawe na matope huko Katesh Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, wameonesha hisia zao za kutoafiki kuishi katika makazi mapya ya eneo lililotengwa na Serikali, wakidai haitasaidia bali itawaumiza kwa kuwakosa wapendwa wao.
Wakizungumza na Dar24 Media, baadhi ya Waathiriwa hao akiwemo Andrea Safari wamesema hali hiyo itawaathiri kwani walikuwa wakiamka na kuwaona watu, lakini sasa wanaona magogo na mawe hivyo ni bora wakaenda kuishi maeneo mengine ili kuepuka kuathirika zaidi kisaikolojia.
“Halafu zinaniijia sura za watu tuliokuwa nao, nakumbuka tulivyoishi tulivyokaa inaumiza sana kwakweli, fikiria hata kama ni wewe wenzako wote wameondoka halafu hata upewe nyumba nzuri ya kuishi wakati wao hawapo inasaidia nini? ni maumivu tu ni bora kwenda mbali waweza hata hisi uliwaacha huko,” alisema.
Hata hivyo, wameipongeza Serikali kwa jinsi ilivyowahudumia na wote waliotoa misaada wakati wa adha hiyo na kusema hawana jinsi ya kushukuru lakini hiyo haitawafanya kuwa sawa hivyo kwa wale ambao watakuwa tayatri kuwa hapo wao hawawazuii kwani kila mtu ana maumivu yake kulingana na pigo alilolipata.
“Angalia hapo ni eneo walilolala ndugu zangu tisa akiwemo mama mzazi nitawezaje mimi, lakini wenzetu wametangulia na sisi tupo hai ni kusudi la MUNGU yapasa tumshukuru kwa yote asante kwa Serikali na wote waliotukimbilia hatuna jinsi, na kinachonishangaza kila mtu anaongea lake, mimi sitarudi tena hapa simuamini mtu,” alisisitiza Safari.
Maporomoko hayo ya Mawe, miti na Matope ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya Watu 89, uharibifu wa mali na miundombinu yalitokea Desemba 3, 2023 ambapo pia kaya 1,150 zenye wakazi wapatao 5,600 ziliathiriwa, ekari 750 za mashamba kuharibiwa, vifo vya mifugo na uharibifu wa mazingira.