Mshambuliaji Mpya wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Joseph Guede ameugomea uongozi wa timu hiyo kuvaa jezi namba tisa ambayo walikuwa wamemwandalia na kuichagua namba 14.
Ofisa Habari wa miamba hiyo ya soka nchini, Ally Kamwe amesema sababu ya kumchagulia namba tisa nikutokana na uwezo wake wa kufunga kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wao aliyetimkia Pyramids FC ya Misri, Fiston Mayele.
“Amekataa namba tisa ambayo tulimuandalia na badala yake ameichagua namba 14 na sababu kubwa ya kuichagua namba hiyo ni kutokana na kumkubali aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry,” amesema Kamwe.
Meneja huyo wa Kitengo cha Habari amesema hawakuwa na namna zaidi ya kukubali ombi lake hilo na amewatahadharisha mabeki na makipa wa timu za Ligi Kuu kujiandaa vizuri kwani amemfuatilia mchezaji huyo mazoezini Avic Town na kubaini vyema uwezo wake.
Amesema Guede ni Mshambuliaji aliyekamilika kila idara ana uwezo wa kufunga kwa kichwa na miguu yote miwili hivyo kwa kupata saini yake wanaamini wamemaliza tatizo la ushambuliaji na kuwafurahisha mashabiki zao.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo inaeleza kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amempa Mshambuliaji huyo majuma mawili ya kumweka sawa kabla ya kuanza kumtumia kwenye mechi za mashindano yote ambayo wanashiriki.
Guede ametua Young Africans akichukua nafasi ya Mshambuliaji Hafiz Konkoni ambaye kiwango hake kilishindwa kumvutia kocha Gamondi na kuamua kumtoa kwa mkopo kwenye klabu ya Dogan Türk Birligi ya Cyprs.