Serikali Nchini, imeanza utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme wa Gridi katika Mkoa wa Rukwa kupitia mradi wa TAZA, ulioanza kutekelezwa Novemba, 2023 unatarajiwa kukamilika Mwezi Agosti, 2026, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa uhakika.

Hayo yamebainishwa hii leo Februari 1, 2024 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Aida Khenani aliyetaka kufahamu mkakati wa kumaliza changamoto ya upatikanaji umeme wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa.

Amesema, kwa sasa Shirika la Umeme Nchini – TANESCO, linaendelea kufanya maboresho ya miundombinu ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme mkoani humo, kwa kujenga kituo kipya cha kupoza umeme.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme nchini, Kapinga amesema upungufu wa umeme unaendelea kushuka kutoka megawati 400 hadi 144 kwa siku ya leo (Februari 1, 2024) na kudai kuwa utekelezaji wa Mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Februari kuelekea Machi 2024 utaanza kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.

Aidha, Kapinga pia amezungumzia kazi ya upelekaji umeme wa gridi Mkoani Katavi na kudai kuwa tayari kuna mradi unaoendelea kutekelezwa na kwa sasa baadhi ya vituo vya kupoza umeme vimekamilika na hivyo, nguvu sasa inawekwa zaidi katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwenda mkoani humo.

Mabadiliko Tabianchi: Serikali kujenga ukuta Nungwi
Guede aigomea Young Africans